Thursday, March 1, 2012

HESLB kuwapeleka kortini waliokaidi kulipa madeni

 

Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiriano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), inatarajia kuwafikisha mahakamani watu ambao hawajarejesha madeni ya fedha walizokopeshwa wakati wakisoma vyuoni.
 Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiriano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, amesema kuwa wanatarajia kuwafikisha mahakamani wale wote ambao hawajarejesha madeni, ingawa hakusema ni lini watafikishwa mahakamani.
amesema kuwa awali walitoa notisi ya siku 21 kuanzia Januari 19, mwaka huu kwa walengwa wote wanaodaiwa na HESLB wawe wamejitokeza na kufika ofisi za bodi.
Aliongeza kuwa, baada ya muda huo kupita bila wadaiwa kujitokeza, wameamua kuwafungulia mashitaka mahakamani.
Aliongeza kuwa mashitaka hayo yatawahusu wanafunzi wote waliosomeshwa na Serikali kupitia HESLB, na haitaangalia ni mwaka gani. Hata hivyo, hakutaja idadi yao.
“Hatuangalii ni mwaka gani, tunachoangalia ni wanafunzi wote waliosomeshwa na Serikali tangu mfumo wa kuwalipia wanafunzi ulipoanzishwa nchini,” amesema Mwaisobwa.
Kuhusu watu wasiokuwa na kazi ambao bado wapo nyumbani hawajapata kazi Mwaisobwa amesema: “Hiyo haijalishi, mkataba unasema utasomeshwa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo mpaka pale utakapomaliza chuo, suala la kupata kazi halipo katika mkataba.”
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...