Singita ndiyo hoteli nambari moja duniani, ikichukua tuzo hiyo kwa mwaka wa pili mfululizo. Tuzo hizo hutolewa kila mwaka na taasisi maarufu ya Marekani, US Travel + Leisure ambayo ‘hudili’ na viwango vya biashara ya utalii duniani.
Hoteli hiyo, inathibitisha kwamba thamani ya Tanzania ipo juu mno, ndiyo maana mwekezaji kutoka Afrika Kusini, Luke Bailes, aliamua kufanya uwekezaji wa hali ya juu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Matokeo hayo, yaliandikwa Agosti mwaka huu kwenye jarida maarufu kwa kuchapisha matukio ya biashara za utalii, linaloitwa T+L Magazine. Jarida hilo linamilikiwa na Taasisi ya US Travel + Leisure.
Tangu kufunguliwa kwake, Singita Grumeti imekuwa kivutio cha viongozi, matajiri na watu maarufu ambao mara kwa mara hutinga kujivinjari, vilevile kujionea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Kwa mujibu wa US Travel + Leisure, sababu ya kuipa Singita hadhi ya kuwa hoteli namba moja duniani, inatokana na muundo wake, huduma zinazotolewa, kuwa ndani ya mbuga kubwa kabisa ya wanyama duniani (Serengeti), vilevile wageni mashuhuri inaopokea.
Inaelezwa kwamba Singita Grumeti ndiyo hoteli inayoongoza kwa sasa duniani kwa kupokea wageni wenye hadhi ya daraja la kwanza, wakiwemo marais, matajiri, wanamichezo, wasanii, viongozi mbalimbali maarufu ulimwenguni na kadhalika.
HAWA WANATAJWA KUJIVINJARI SINGITA
Marais wa 42 na 43 nchini Marekani, Bill Clinton na George W. Bush, kwa nyakati tofauti wamefikia kwenye hoteli hiyo baada ya kuvutiwa na sifa zake zinazotikisa duniani.
Bilionea wa Kirusi anayemiliki Klabu ya Chelsea ya Uingereza, Roman Abramovich, alipotembelea nchini Septemba 2009, inaelezwa kwamba alilala kwenye hoteli hiyo.
Bilionea wa Kihindi, Mukesh Ambani ambaye kwa sasa ni tajiri namba 19 duniani, alifika nchini mwaka jana na kufikia kwenye hoteli hiyo.
Wakati alipowasili nchini, Mekesh alikuwa tajiri namba nne duniani. Ripoti ya mwaka 2011, ilimtaja kuwa tajiri namba tisa na sasa anashika nafasi ya 19.
Mke wa zamani wa mwanasoka anayechezea Chelsea ya England, Ashley Cole, Cheryl, alipofika nchini miaka miwili iliyopita, inaelezwa pia kwamba alifikia kwenye hoteli hiyo.
Mwanamitindo aliye pia mcheza sinema maarufu wa Hollywood, Marekani, Angelina Jolie na mumewe Brad Pitt, waliripotiwa kufika nchini na moja kwa moja makazi yao yakawa Singita Grumeti.
Wengine ambao wanatajwa kuwahi kupumzika kwenye hoteli hiyo ni mwanamuziki wa Marekani, Sean Carter ‘Jay Z’, mwanasoka Thierry Henry, Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa orodha ya wageni wanaofikia Singita ni kubwa mno, tatizo hufanywa siri kwa sababu watu wengi mashuhuri ulimwenguni huwa hawapendi ijulikane kama wamefikia kwenye hoteli hiyo kwa sababu za kiusalama.
SIFA ZA HOTELI HIYO
Ni hoteli yenye eneo kubwa, kutoka ‘loji’ moja hadi nyingine, inabidi utumie usafiri maalum.
Imegawanywa kwenye ‘loji’ mbili, moja inaitwa Ebony na nyingine ni Boulder.
Hoteli hiyo, pia inaundwa na ‘loji’ nyingine inayoitwa Castleton Camp ambayo inaweza kuhamishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Bei ya chini kabisa kwa mtu kulala kwenye hoteli hiyo ni shilingi 2,000,000 na bei hiyo hutegemea na msimu.
Bei zimetofautiana kati ya ‘loji’ moja hadi nyingine na mtu kulala kwenye Castleton Camp, inaweza kugharimu mpaka shilingi milioni 23 kwa siku moja.
Singita Grumeti ni moja kati ya hoteli za Singita za nchini Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment